Monday, November 18, 2013

FREDDY SUPREME NA ORCHESTRA FAUVETTE JUNE 1970

Marehemu Freddy Supreme Ndala kasheba na King Kiki


Orchestre Fauvette

June 1970 kulikuweko na kipindi RTD kilichoitwa  NI MASHUHURI, kipindi hiki kilikuwa kikiendeshwa na binti aliyeitwa wakati huo Eddah William. Na katika kipindi kimoja wapo mwezi huo, Eddah alimuhoji mwanamuziki aliyeitwa Freddy Supreme. Wote wawili baadae walibadili majina, Eddah William alikuja kuwa Eddah Sanga, na Freddy Supreme alikuja fahamika kwa jina la Ndala Kasheba. Siku hiyo Freddy alikuwa studio akihojiwa kuhusu bendi aliyokuwa akiingoza wakati huo ikiitwa Orchestra Fauvette, bendi aliyoiongoza toka kuanzishwa kwake.
Freddy alianza kueleza kuwa yeye alianza kufundishwa gitaa na baba yake wakati akiwa na umri wa miaka 12. Baba yake alijua kupiga gitaa japo hakufanya kazi ya uanamuziki, alikuwa akipiga gitaa nyumbani baada ya saa za kazi. Freddy aliamua kuacha kazi ili afanye kazi ya muziki na ndio ilikuja kuwa kazi yake mpaka alipofariki.
Freddy alieleza kuwa bendi ya Orchestra Fauvette ilianza tarehe 7 mwezi wa sita mwaka 1964 katika jiji la Lubumbashi huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Jina hilo Fauvette kwa kiswahili ni Chiriku, bendi ilikuwa na muimbaji ambaye waliamini alikuwa anaimba kama chiriku na hivyo kuipa bendi hiyo jina hilo. Vyombo vyao vya muziki walinunua Ujerumani kupitia duka la muziki la Dar es salaam Music House (duka lipo mpaka leo). Vyombo vilikuwa  vya aina ya Hofner, jina lililoheshimika sana kwa wanamuziki wakati huo.

Picha hapo juu ni za magitaa ya Hofner yalikuwa mazito kuyabeba lakini yalikuwa imara na yenye sauti nzuri sana.
Kati ya nyimbo ambazo zilipigwa katika kipindi hicho ni Camarade ya nzela..ambayo Freddy alieleza ni wimbo uliokuwa ukizungumzia rafiki wa kukutana nae barabarani au njiani, ambaye roho yake huwa kama sanduku la nguo, ambalo ndani yake huwezi kujua kuna nini. Pia ulipigwa wimbo Jacqueline ambao ulitungwa na mwenyewe Freddy ambao alieleza alikuwa kamtungia mpenzi wake aliyempenda Jacqueline. Wimbo mwingine uliopigwa katika kipindi hicho ni Nono na Kalemie, wimbo huu ulitunguiwa binti aliyeitwa Nono mkazi wa Kalemie ambaye alikuwa mpenzi mkubwa wa bendi ya Fauvette.
Fauvette ilifika Dar na kuwa inapiga katika ukumbi wa White House Ubungo, lakini kwa miaka hiyo Ubungo ilikuwa mbali sana na mji, na kulikuwa na ajali nyingi zikiwapata wapenzi wa bendi katika usafiri wa kutoka kwenye muziki, hivyo bendi ikaamua kuhamia ukumbi wa Mikumi Tours ambapo walikuwa wakipiga Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Fauvette walikuwa na ndoto ya kuwa bendi bora Afrika. Hawakufikia huko lakini waliweza kuweka alama kubwa katika historia ya muziki wa Afrika mashariki na Kati

1 comment: