Saturday, August 4, 2012

The Great Western Jazz



 
Kadri ya maelezo yake mwenyewe, Mzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi maarufu ya Western Jazz. Mzee Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia mara nyingine walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.
Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, kwa taratibu hizo watu wa sehemu mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika.
Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi ya Tanganyika wakati huo, na kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha bendi na kuiita Western Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake, ilikuwa ni Dar es Salaam Jazz Band peke yake iliokuwa na gitaa ya umeme, na hivyo Nhende akawa na kazi ya kutafuta mpigaji kwa ajili ya bendi yake. Ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde (Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band  iliyokuwa chini ya Mzee Muba, baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga Jazz Band, wakati huo pia  chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam tawi lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae Nhende alipata transfer ya kikazi na kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo) mpiga Saxaphone toka Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz, ukiangalia habari ambayo imeandikwa katika blog hii iliyohusu Dodoma Jazz, unapata mtiririko wa wanamuziki hawa waliotoka Tabora Jazz, mmoja wao Rashid Hanzuruni alitua kwa muda Dodoma. Pamoja na Rashid Hanzuruni pia walisindikizana na Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana aliyoifanya katika anga za muziki, Hanzuruni nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western. Pamoja na kuwa mpigaji mzuri sana wa solo, tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana Shamba Abdallah akachukua nafasi, solo la Shamba linasikika kwenye nyimbo kama Rosa na Vigerege.
Ukumbi wa  nyumbani la Western Jazz ulikuwa Alexander Hall, ukumbi ambao hatimae ulikuja kuwa ukumbi wa DDC Kariakoo. Western Jazz walinunua drums zao za kwanza baada ya Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha zikiwa juu ya gari lao kwenye ukumbi wa Western Jazz. Western walijibu mapigo kwa kwenda kununua seti ya drum  toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers.
Western Jazz Band walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya, na kwa miaka mngi bendi hii ilikuwa maaruf sana Afrika ya Mashariki nzima. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.
Rashid Hanzuruni, kama ilivyo watu wote walio mahiri katika vyombo vyao vya muziki alilipenda gitaa lake na alifanya mazoezi kila alipopata muda. Kwa maelezo ya mtu aliyekuwa karibu nae alisema huyu bwana kuna wakati dansi likishaisha wenzie wakienda kulala yeye aliwasha tena mashine na kuanza mazoezi ya gitaa. Kuna hadithi ambayo hata mimi niliiamini kwa miaka mingi kuwa Doctor Nico alipokuja Tanzania alimuulizia Hanzuruni, hadithi hii si ya kweli. Kwa malezo ya mtu aliyekuweko kipindi hicho, Western Jazz walialikwa kupiga pamoja na Dr Nico alipokuja Tanzania kati ya mwaka 66 na 67, na katika maonyesho hayo, ndipo kwa mara ya kwanza Hanzuruni  alimuona Dr Nico kwa karibu na kupenda staili ya upigaji wake, na pia ndipo alipomuona Dr Nico akipiga Hawaian Guitar, nae akalipenda sana gitaa hilo na Western Jazz wakalinunua na Hanzuruni akawa mpigaji maarufu wa gitaa la hawaian, baada ya hapo Hanzuruni alifanya sana mazoezi ili aweze kupiga gitaa kama Dr Nico. Ni vizuri kulisema hapa kuwa Hanzuruni ndie alikuwa mwanamuziki aliyelipwa vizuri kuliko mwanamuziki yoyote wa Dar Es Salaam wa aina yake, katika kipindi hicho.



No comments:

Post a Comment