THE JETS

THE JETS
THE JETS

PAKUA HII

Alhamisi, 2 Agosti 2012

Ramadhan Kinguti aka Kinguti SystemRamadhan Maulid Kinguti maarufu kama Kinguti System ni mzaliwa Ujiji, Kigoma.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Super Kibisa iliyokuwa na makao yake makuu Kigoma. Super Kibisa  iliyoanziswa 1968 na Kinguti akajiunga nayo mwaka 1977, katika kipindi hicho kiongozi wa bendi alikuwa Mlolwa Mussa Mahango ambaye alikuwa ni binamu yake Ramadhani Kinguti, hivyo ikawa rahisi kidogo kwake kujiunga na bendi ile. Bendi ilikuwa mali ya watu watatu, Gollo Saidi, Haruna Mahepe, na Maulidi. Mapema kabisa kipaji chake cha kutunga kilianza kujitokeza na aliweza kutunga nyimbo kadhaa kama vile Kazi ni uhai, Mapenzi tabu,na Zaina.
Mwaka 1979 alichukuliwa na Ahmed Sululu ambae alikua katibu wa Dodoma International na kuhamia Dodoma, Dodoma International ilibidi wamchukue Kinguti kujaza nafasi ya Shaaban Dede ambaye alikuwa kahama Dodoma International na kuhamia JUWATA. Katika bendi hiyo alikutana kwa mara ya kwanza na mpiga gitaa mahiri marehemu Kassim Rashid. Baada ya hapo alihamia Orchestra Makassy ambapo wakati huo walikuweko wanamuziki akina Marehemu Masiya Radi mwimbaji ambaye alifariki kwa kukanyagwa na daladala maeneo ya Kinondoni Mbuyuni, Doctor Remmy, Andy Swebe, Keppy Kiombile, John Kitime, Issa Nundu, Kyanga Songa, Choyo Godjero na wengineo, pia alikuweko Mzee Aimala Mbutu kwenye solo, na Kassim Mganga (babake wa mwanamuziki wa Bongo flava Kassim Mganga-Milionea wa Mahaba) kwenye rhythm, na wengine wengi. 1986 alijiunga Afrisongoma chini ya Lovy Longomba, hapa alitunga nyimbo kadhaa kama Pesa ni maua, Amana mpenzi, Estah Usituchonganishe, waimbaji wakati huo walikuwa Kinguti, Lovy Longomba  na Anania Ngoliga, kwenye solo alikuweko mzee Kassim Mponda, na rhythm Maneno Uvuruge. Kwa muda mfupi alikuwa DDC Mlimani Park, na hapa akatunga kile kibao maarufu Visa vya mwenye nyumba, ambapo aliimba na Hassan Bitchuka, Francis Lubua, Hussein Jumbe na Benno Villa. Mwaka 1989 alikuwa moja ya wanamuziki waanzilishi wa Bicco Stars Band akiwa na Mafumu Bilali, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mzee Aimala Mbutu, walitikisa na vibao kama Muuza chips, Leyla, Magreth maggie, Kitambaa cha kichwa, Nyumba ya kifahari, na nyingine nyingi tu. 1999 alijiunga na kilimanjaro Connection, alikaa bendi hii iliyokuwa chini ya Kanku Kelly kwa miaka miwili kisha kuanzisha bendi akiwa na Hassan Shaw, bendi iliyoitwa The Jambo Survivors ambayo wengi hapa Tanzania wataikumbuka kwa kibao cha Maproso. Bendi ya Jambo Survivors ikiwa bado na Ramadhan Kinguti na Hassan Shaw, kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ni bendi ya Kitanzania iliyo na makao  nchini Thailand


Maoni 3 :

malika alisema ...

hongera baba kwa kutuhabarisha za long,mimi nina ombi,kulikuwa kuna band inaitwa zaita musica chini ya marehemu ndala kasheba,kulikuwa kuna wanamuziki kama defrea,seleman na wengine wengi,ombi langu ni kujua seleman yupo wapi,alikuwa anapiga chombo kinachoitwa saxphone kama sijakosea

Kisondella, A.A alisema ...

Hili gogoro la kuama na nyimbo ambapo bendi ya DDC Mlimani Park ni mdau mkubwa.

Nakumbuka wimbo wa Visa vya wenye Nyumba kutungwa na Ramadhani Kinguti kabla hujashika kasi Sikinde, Kinguti aliama kwenda Bicco Star na kwenda nao. Lakini huku nyuma Sikinde haraka haraka wakaurekodi ule wimbo. Mwisho wa siku kukawa na nyimbo mbili "Visa vya wenye nyumba" wa Sikinde na ule wa Bicco.

Kama hiyo aitoshi Hussein Jumbe alipokuwa Sikinde alitunga wimbo wa "Nani Kaiona Kesho" ule wiombo ulikuwa unaimbwa vizuri kila mwanamuziki akiimba kipande chake. Lakini Husseni Jumbe alipoama kwenda TOT akaama na wimbo wake. Huku nyuma Sikinde wakabadilisha jina na kuitwa Huruma kwa Wagonjwa ukiimbwa vizuri na Marehemu Tino Masinge, Hassan Kunyata, Shabani Dede Benno Villa Anthony na Hassan Bitchuka. Jumbe akaendelea na wimbo wake TOT akiuimba na wanamuziki aliowakuta kule.

Katika nyimbo zote hizi Benno Villa ndiye mtaalamu wa ku-model maneno. Sijaelewa nani nakuwa ameishiwa nyimbo yule aliyeondoka na wimbo wake au aliyeachiwa.

Kisondella (Mafinga-Iringa)

Kisondella, A.A alisema ...

Namkumbuka na nilimkubali sana pale alipokuwa anaimba sambamba na Marehemu Lovy Longomba - Sauti nene ya kinguti ilikuwa inawiva sawia na sauti kali nyembamba ya kupanda ya Marehemu Lovy Longomba. Hii inafanya nilinganishe matching za Bitchuka na Gurumo, au Bitchuka na Max Bushoke au Hamisi Juma na Cosmas (Pale Sikinde) au Pale Vijana Jazz combination ya Hamisi na Jerry Nashion au Maneti na Jerry Nashion au Eddy Sheggy na Adamu Bakari au Pale Bima Lee combination ya Athumani Momba na Jerry Nashion and Athumani Momba na Roy Bashekanako.

Kisondella (Mafinga-Iringa)