Tuesday, April 3, 2012

Historia ya Simba wa Nyika na matawi yake


Asili ya Simba wa Nyika ni Jamhuri Jazz band, bendi iliyokuwa na makao makuu yake Tanga ambayo ilianza niaka ya 50. Katika  miaka ya 60 na 70 Jamhuri Jazz Band hii ilikuja juu sana katika anga za muziki wa Afrika ya Mashariki. Ikiwa na upigaji wake ambao ulikuwa wa kipekee na kuifanya iwe na nembo ya aina ya peke yake kimuziki. Katika miaka ya sabini pamoja na wanamuziki wengine walikuwemo wanamuziki ndugu Wilson Peteraliyekuwa anapiga solo guitar na George Peter, aliyekuwa mpiga bezi mahiri na hata kupewa jina ‘Mtoto Joji’. Bendi ilikuwa na waimbaji mahiri Rajab Khalfani na Yusuf Mhando, mpiga rhythm alikuwa Harrison Siwale aka Satchmo, huyu alikuwa na upigaji wa rhythm wa aina ya peke yake ambao haujaigwa mpaka leo popote, upigaji huo unaweza kusikika katika nyimbo za Jamhuri kama vile Shingo ya Upanga, Mganga na 1 na 2, katika wimbo wa Mganga na 2 gitaa hilo lililkuwa likisikika katika wimbo uliokuwa ukitumika kutambulisha mwanzo wa kipindi cha ‘Jioni Njema’ katika radio ya RTD miaka hiyo.   
Wilson na George walikuwa na ndugu zao wengine akiwemo dada yao Maria na mdogo wao ambae pia alikuwa mwanamuziki  William. Baba yao Mzee Peter asili yake ni kutoka Burundi na alihamia Hale Tanga katika kipindi ambacho wageni wengi walihamia Tanga kufuata ajira katika mashamba ya mkonge. Wakati akihamia Tanga, Wilson alikuwa amekwishazaliwa, lakini wadogo zake walizaliwa Pongwe huko Tanga, Mzee Peter aliendelea kufanya kazi ya udereva wa malori mpaka miaka ya themanini. Huku mdogo wao William alianza kufahamika zaidi Mombasa kwa kuwa mpiga drum na tumba  mahiri na hata katika baadhi ya nyimbo za kaka zake aliwahi kurekodi, lakini bahati mbaya katika miaka ya 80 alipata maradhi ya akili na kushindwa kuendelea kupiga muziki, japo inasemekana bado yu hai Nairobi akitunzwa na watoto wa Wilson.
Mwanzoni mwa miaka ya 70, Wilson na George  Peter wakiwa na wanamuziki wenzao wengine kama Elias John –Luza, walihama Tanga na kuingia Arusha na kuanzisha bendi ya Arusha jazz. Inasemekana walikuwa pia wahame na Harrison Siwale lakini haijulikani kwa nini dakika za mwisho akabadili mawazo na kuendelea na Jamhuri Jazz Band. Arusha jazz Band ilirekodi nyimbo zao za kwanza na katika recordings hizi William pia alishiriki na walirekodi nyimbo kama Mary Mtoto, Mama Suzie, Tutengane Salama.
 Na kwa kweli wengi waliokuwa wapenzi wa muziki Arusha 1973 watakumbuka madansi ya mchana ya bendi hii wakati huo. Mwaka 1974 bendi ikavuka mpaka na kuingia Kenya kwa kupitia Mombasa. Huko wakaongezeka wanamuziki wengine kama Tom Malanga(Mpiga bezi), huyu alikuwa mwananchi wa Kenya, Mrabai. Pia alijiunga Rashid Juma(Drums), Haidary Hafidh(Tumba) huyu alikuwa Mgunya wa huko Mombasa. Bendi ilipokuwa Mombasa ikaanza kuitwa Simba wa Nyika, ikiwa ni muendelezo wa staili ya kujiita Wanyika iliyoanzia Arusha. Kuna hadithi moja kuwa walianza kujiita Wanyika kutokana na mashati fulani walionunua yaliyokuwa na picha ya simba yuko katika nyika.
Klabu ya kwanza kwa bendi hii kupiga kule Mombasa ilikuwa Sports View, na hapo ndipo bendi ilipoanza kupata umaarufu, na ilikaa mji huu mpaka 1975, ambapo ilihamia Nairobi na kuanza mambo yaliyoitambulisha katika ulimwengu wa muziki…….inaendelea


3 comments:

  1. NAISUBIRI MPAKA MWISHO,HAWA GEORGE NA WILSON PETER NASIKIA NDIO CHANZO CHA MAREHEMU TX MOSHI KUWA MUIMBAJI KWANI ALIUPENDA MUZIKI NA KUJIFUNZA KUPITIA KWA KAKA ZAKE HAO AMBAO WOTE PAMOJA NA TX WANATOKA HALE,HATA UIMBAJI WA MOSHI UKIUSIKILIZA NI KAMA WA LES WANYIKA.

    SENETA WA MSONDO,REVERE,BOSTON,MASSACHUSSETTS,USA

    ReplyDelete
  2. Seneta wa Msondo,unayosema ni kweli marehemu Tx Moshi William alikuwa akisema wazi mbele ya akina George na Wilson kuwa uimbaji wake anafuata technics au njia za Geoge kwa vile alipendelea sana uimbaji huo wa George,Mara nyingi Tx alipokuwa likizo hasa mwezi wa ramadhani alikuwa akitutembelea Nairobi na kuwa pamoja nae hadi anaporudi Dar,kwa hiyo usemi wako seneta ni kweli kabisa.
    Abbu Omar,Prof.Jnr(Mwanamuziki)Tokyo,Japan.

    ReplyDelete
  3. Naomba historia ya mpiga Tumba wa Simba wa Nyika Haidary Hafidh.

    ReplyDelete