Friday, October 29, 2010

Muziki wa Taarab





Taarab ina historia ndefu katika muziki wa Tanzania kama ulivyokuwa muziki wa dansi. Wapenzi wa taarbu wa zamani waliiweka taarabu katika vyanzo kama Taarab ya Tanga, Taarab ya Dar es Salaam,Taarab ya Zanzibar na Taarab ya Mombasa. Taarab ya Zanzibar wakati huo ilikuwa ni ile yenye kundi kubwa la wanamuziki, kwa kufuata mfumo wa muziki huo kama ulivyokuwa ukipigwa huko Misri. Historia inatueleza kuwa Sultan  Sayyid Barghash wa Zanzibar kwenye mwaka 1870, alipeleka wanamuziki wake wawili kwenda Misri kupata taaluma ya upigaji wa Taarab , na waliporudi ndipo mwaka 1905 wakaanzisha klab ya Ikwaan Safaa, kundi ambalo pamoja na kupitia misukosuko mingi ya kisanii na hata kisiasa, lipo mpaka leo. Na muziki wa kundi hili na makundi mengine yalifuata aina hii ya muziki kwa muda mrefu, ulikuwa unajumuisha kundi kubwa la wanamuziki wenye vifaa mbalimbali kitaalam wanaweza kuitwa orchestra.  Taarab ya Dar es Salaam haikupishana sana na ile ya Zanzibar wakati huo, hapa Dar kukiwa na vikundi kama Egyptian Musical Club na Alwatan Musical Club vilivyoanza tangu kwenye miaka ya 30. Mombasa ilijulikana sana kwa aina yake ya Taarab iliyofanywa maarufu na akina Juma Bhalo waliokuja na upigaji ulioiga mipigo ya muziki wa kihindi, uliopata umaarifi kutokana na sinema za kihindi. Ukisikiliza nyimbo maarufu za Juma Bhalo kama Pete, utasikia uimbaji upigaji na upangaji zauti unaofanana sana na muziki wa kihindi. Taarab ya Tanga kwa kweli ndio ilistahili kuitwa modern taarab, taarab hii ndio ilikuwa ya kwanza kuanza kuingiza vifaa ambavyo vilikuwa vigeni katika taarabu, magitaa, akodian , na mipigo ya ngoma za kiasili, na pia vikundi vya Tanga vilikuwa vidogo vikiwa na washirika wa wastani wa watu kumi na mbili. Kazi za Black Star na Lucky Star wengi tunazijua na waimbaji wake maarufu kama Bi Shakila, Hasmahani sauti zao zilitawala anga ya muziki huu katika miaka ya sabini..
Katika anga za leo kuna vikundi vingi vinavyotangaza vinapiga muziki wa taarabu, jambo ambalo limepingwa na wengi kuwa kinachopigwa pigwa sasa si taarabu, kuna hata waliofikia kusema kwa vyovyote vile kinachoitwa  mipasho hakina uhusiano wowote na taarab!!

2 comments:

  1. HUITAJI KUWA MWANAMUZIKI AU MTAALAMU WA MUZIKI KUJUA KWAMBA HIKI KINACHODAIWA KUWA TAARABU 'MIPASHO' SIYO TAARABU. UKWELI NI KWAMBA KUNA UPUNGUFU WA UBUNIFU KWA WANAMUZIKI WA 'MIPASHO' KUPATA JINA LA MTINDO WA MUZIKI WAO. KILICHOBAKI NI KUDANDIA NA KUHARIBU MTINDO WA TAARABU. USHAURI KWA WANA 'MIPASHO': UPENI JINA MTINDO WENU!!

    ReplyDelete
  2. Taarabu ya sasa haina tofauti sana ba bongo fleva, ukizungumzia mziki. Ni labda tuite `maboresho' lakini ndio yanaharibu kiini na sili ya kile kitu.
    Kwa mfano taarabu, manake kwa mimi niuavyo ni mziki wa kistaarabu, kwamba unaimbwa na watu wanausikiliza na wanas tarehe, lakini hauvunji ile hali ya `kitsraabu' kama sasa wafanyavyo!
    Lakini tukubali kuwa kuna mabadiliko kuna kwenda n wakati na hasa katika kuivutia hadhira, hasa katika maslahi. Kwani kinachogomba ni nini, ni maslahi, kama usipoimba uchi nani atakuja kwako, kama usipokatika, ....kama usipofanya vile hutapata wateja, na wateja wenyewe siunawajua!
    Twashukuru sana mtaalamu. Mimi nitakuita mtaalam, kwasababu unatupa mambo yaliyokuwa yanasahaulika, ...mungu akuzidishie kwa ukarimu wako huo!

    ReplyDelete